Tanzania jarida Desemba 2016

Wapendwa marafiki,
Tunapomaliza mwaka 2016 hebu tuzamishe nafsi zetu katika tafakari ya kauli zifuatazo: “Umaskini haukuletwa na Mungu, bali unasababishwa na binadamu kwa sababu walionacho hawagawani na wasionacho”. Hii ni kauli ya mama Theresa wa Kalkuta. “Umaskini uliokithiri ni kazi ya wanadamu na ni wanadamu pekee wanaoweza kuutokomeza”. Kauli ya Joseph Wresinski muasisi wa ATD. Uchoyo, ubinafsi, kujilimbikizia mali na mengine ya namna hiyo yamekuwa chanzo cha vita, vurugu, uharibifu wa mazingira na zaidi janga la umaskini ambalo ni uvunjifu wa haki za binadamu.

Sisi wana ATD tukishirikiana na wadau wengine ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba hawa wanarejeshewa utu na heshima yao na hivyo kwamba waweze kusimama na kusonga mbele kuleta maendeleo yao binafsi na katika jamii. Umoja wetu, ushiriki wetu na kujitoa kwetu sisi ni muhimu kwa sababu sisi tunabaki kuwepo wakati wana timu hubadilika kila baada ya muda. Ni jukumu letu kujenga jamii inayojiamini na iliyo tayari kushiriki kuleta maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla.

Mwaka huu wa 2016 umekuwa wa mafanikio kwetu sote kama shirika. Tumeshiriki katika shughuri mbalimbali na tafiti na hivyo kujenga mahusiano zaidi. Hii imejiakisi katika maadhimisho ya Oktoba 17 ambayo yalifana kote, Dar, Njombe na Dodoma. Washirika walitoka katika nyanja mbalimbali, wanataaluma, wawakilishi kutoka serikalini na mashirika mbalimbali.Kimataifa tumeshiriki katika mkutano wa Bangui Afrika ya Kati, na tunatarajia kushiriki katika mkutano wa Dakar kule Senegal. Yote hii ni katika maadhimisho muhimu ya mwaka 2017: miaka 100 ya kuzaliwa Wresinski, miaka 60 ya kuanzishwa shirika, miaka 30 ya kuadhimisha Oktoba 17. Yote haya ni wajibu wetu na tunapaswa kujitoa kwa dhati.

Niwatakie Krismasi njema na Heri ya mwaka mpya.
Aslaam Aleykum,
Constantine S. Munema.

Kuendelea kusoma jarida hili, download PDF.