Barclay na Cyndie

Photo above: CAR, 2007, Uwani kwa ATD Dunia ya Nne Bangui – AR0200901002  © Jacqueline Page

Makala hii imetayarishwa na Niek Tweehuijsen mfanyakazi wa kujitolea wa  ATD Dunia ya Nne.

Katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kama ilivyo katika nchi nyingi siyo kila mmoja anaweza kuishi mahali palipo salama. Hususan wale waliogubikwa na ufukara, hawana uchaguzi zaidi ya kuishia katika makazi yaliyo hatarishi yanayokabiliwa na mafuriko na yakiwa yameathirika kwa uchafuzi wa mazingira.

Barclay, mkewe Cyndie pamoja na watoto wao wawili wamechoka kuishi katika ‘eneo’ hatarishi. Ni kawaida kwa waasi na vikundi “vinavyojihami” kufyaturiana risasi mara kwa mara kwa muda wa miaka kadhaa katika eneo hili. Vikundi hivyo pia huchoma moto biashara za wale wasiokubali kulipia ada ya “ulinzi”. Makundi haya huua bila huruma na yameweza kufarakanisha jumuiya za Wakristu na Waislamu wenyewe kwa wenyewe. Hata leo wakazi wa eneo hili wanaishi kwa tahadhari wakiogopa kupigwa risasi zilizopoteza mwelekeo.

Hata hivyo Barclay na familia yake walifanikiwa kutoroka katika eneo hilo na kwenda kufanya makazi katika kingo za mto Oubagui, mto unaotiririka kupitia katikati ya mji mkuu. Barclay alipata chumba mahali ambapo familia yake inaweza kuishi kwa usalama. Kodi ya pango ilikuwa katika uwezo wao. Ulikuwa kama mwanzo mpya. Lakini matumaini haya yalikuwa ya muda mfupi. Wakati wa kipindi cha mvua mto ulifurika hadi katika makazi yao mapya. Maji yalibubujika  moja kwa moja kutoka chini katika sakafu ya maji.

  • Cha kusikitisha ni kwamba hayo mafuriko yalikuwa yanatabirika. Mto Oubangui hufurika mara moja kila baada ya miaka kumi. Lakini kwa kiwango kikubwa janga la wakati huu lilionesha ishara wazi za mabadiliko ya tabia nchi. Wataalamu walifafanua kwamba mafurikao yalitokana na idadi ya sababu.ambazo hatimaye zote kwa pamoja ziliungana pamoja na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.
Bangui, 2007, akikata minazi AR0200901097 © Jacqueline Page

Ukataji wa miti usiodhibitiwa ambao mara kwa mara ulikuwa ukitekelezwa katika mazingira yaliyojaa mashaka, umesababisha uwiano dhaifu wa mazingira ya asili katika eneo hilo. Kila mwaka mamia ya miti ya kale ikiwa imelazwa katika malori makubwa huhamishwa nchini katika misafara mirefu isiyo na ukomo. Malighafi hizi mbichi husafirishwa nje ya mipaka ya nchi kutajirisha uchumi wa mataifa mengine kwa gharama za Jamhuri ya Afrika ya Kati. Miti mingine huchomwa au kukatwa kwa ajili ya mkaa na kuni. Taratibu misitu inapotea. Wakihatarishwa na uoto wa asili unaofifia, wanyama wanahama na kutafuta makazi katika maeneo mengine. Mito pia imeharibiwa. Baadhi inaelekezwa kutoka katika njia zake za asili kumwagilia migodi ya dhahabu na almasi. Mingine inachafuliwa kwa kemikali zinazotumika katika migodi. Samaki, wadudu na wanyama wengine wadogo hufa kimya kimya.

Watu waliokuwa wanategemea maisha yao kutokana na kazi ngumu na ambao ndio waliokuwa wanawajibika na utunzaji wa ardhi wamekuwa maskini. Kila anayeweza anaondoka kwenda mjini au katika jiji kujitafutia maisha. Huko wengi wao huishia kuwa fukara wakubwa. Penginepo, migodi huchukua wakazi katika maeneo yanayoizunguka, wakazi ambao huishia kuwa wahanga wa unyonywaji mkubwa wa makampuni. Wakidanganywa na mafanikio ya baadhi yao wachache, wafanyakazi wa migodi huishia kuangamizwa na magonjwa na vurugu. Utajiri wa asili wa nchi umekuwa laana, ukiwavuta wenye madaraka na uwezo kufanya uporaji na rushwa.

Mabadiliko ya tabia nchi na ulafi wa wanadamu –hizi siyo hadithi unazosikia. Barclay na familia yake wameteseka kutokana na matokeo ya madhara ya ubaya unaodhalilisha  sayari hii na kuwagawanya wanadamu.

Pamoja na wakazi wengine  Barclay alijaribu kudhibiti maji ya mto yaliyokuwa yanaongezeka. Alifikiria labda angeweza kuilinda familia yake isidhurike kwa homa ya malaria au homa ya matumbo kutokana na maji machafu ya mto yaliyokuwa yanachafuliwa na vyoo vinavyotiririka na matanki ya majitaka. Lakini muda si mrefu ilikuwa wazi kwamba watalazimika kuhama. Maji yaliingia katika nyumba yao kwa kasi. Barclay na Cyindie waliweza tu kuokoa watoto wao, baadhi ya samani na godoro. Wakiwa wamekata tamaa waliangalia mafanikio yao yakizama. Waliangalia kioski chao kidogo ambamo Cyndie alikuwa akiuza sabuni na vyakula kikielea kitupu katika ziwa dogo lililotokana na mafuriko. Faida iliyotokana na kioski hicho ilikuwa inaweza kuchangia pato la familia pale ambapo pato la Barclay lilipokuwa halitoshi.

Bangui, 1993, Mandhali ya mtaa, rangi ya maji – AR0204101009 ATD Quart Monde © Yves Quetin
  • Katika umri wa miaka 27 Barclay ni mchapakazi asiyechoka. Akiwa na mkokoteni wake alivuka huku na huko katika mitaa ya Bangui kila kukicha akikusanya takataka kutoka  makazi ya wenyeji. Wenyeji walimlipa pesa kidogo kuondoa takataka alizokwenda kuzitupa katika dampo la taka. Kazi yake ilikuwa  muhimu kwa sababu ilimaanisha kwamba watu hawatachoma takataka mbele ya makazi yao hususan plastiki ambazo hutoa gesi yenye sumu inayosababisha magonjwa ya kupumua kwa watoto wadogo. Barclay ananatafuta namna ya kuwafanya watu waelewe ubaya wa madhara haya; watu watafaidika kwa kuelewa hatari ya madhara hayo. Hii kazi ni ya muhimu kwake! Inamwezesha Barclay kuitegemeza familia yake kwa unyenyekevu na kwa heshima. Shukrani kwa kazi hii, ameweza kupeleka watoto wake shule na kumjengea Cyndie kioski kingine hali iliyoimarisha uchumi wa familia.

Watakwenda wapi sasa wakiwa na pesa kidogo katika mifuko yao? Maeneo wanayoyafahamu vema ni kule walikoondoka wakikimbia vurugu. Basi, waliamua kurejea tena huko. “Kwa muda tu”, walijiambia. Lakini hawakuweza kuwasajili watoto wao shuleni au hata kuweka pesa ya kutosha kuanzisha tena biashara. Maisha yao ni magumu zaidi kuliko yalivyokuwa. Cyndie anaumia kwa kuwa hawezi kuchangia katika pato la familia.

Barclay amerudi pale alipoanzia. Lakini anajiona bado kuwa mwenye bahati.

”Familia zingine zilizogubikwa na janga hilo bado zinaishi chini ya maturubai katika kambi za muda. Nitayapitia haya bila kusubiri msaada ambao unaweza usije. Siku moja wanangu watarudi shuleni. Siku moja nitaishi na familia yangu mahali salama. Sikubali kushindwa.”

Baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yalikuja kutoa misaada katika eneo lililoathiriwa na mafuriko. Radio moja ya kimataifa ilichangisha pesa. Lakini familia ya Barcay haikufaidika na msaada huo kwa sababu walikuwa hawaishi tena katika eneo la mafuriko, vilevile hawakuwepo tena katika orodha ya wahanga. Aidha hawatahesabiwa tena katika takwimu na ndivyo ilivyo kwa mamia ya familia zingine.

  • Barclay anaendelea na kazi yake, akichangia alichoweza katika kusafisha mazingira yanayomzunguka. Wakati baadhi wakiichukulia kuwa shughuri isiyo na manufaa – kukusanya takataka na kuzirejesha kuwa zenye manufaa tena –  yeye anaangalia manufaa kwa jumuiya na hicho kinampa majivuno.

Familia yake ilibaki kuwa na bidii. Licha ya mahangaiko yote walikuwa hawajakata tamaa. Wakijitegemea, walikuwa wanatafakari mikakati ya kuendelea kuishi. Hata hivyo swali moja linaendelea kumsumbua Barclay: atalipaje ada za kuwasajili watoto wake? Tayari ameshalipia ada katika shule ingine kando ya mto akiwa amejitoa kwa gharama ya mahangaiko makubwa.

Mabadiliko ya tabia nchi – athari na madhara yake- moja kwa moja yanaathiri familia ya Barclay na mamilioni mengine ya familia duniani kote. Hawana chaguo  zaidi ya kuishi katika mazingira machafu, yanayokabiliwa na vimbunga, mafuriko na mmomonyoko wa udongo wa mara kwa mara. Ili kuishi lazima wafanye kazi hatarishi bila kinga dhidi ya magonjwa, ajali na athari za mwili kuzeeka mapema. Wanalazimika kuishi kwa kula vyakula vya viwandani vilivyotengenezwa kwa kemikali,

Bado pamoja na yote haya, familia zinazoea, zinapambana na kustahimili, zikitembea vichwa juu. Mara zote wakiwa katika mazingira ya kufa na kupona, macho yao yakiwa yamekazwa mbele katika upeo wa macho na hufanya kila kinachowezekana katika uwezo wao kufanya hatima ya watoto wao iwe tofauti na wanayopambana leo. Wao kwa wao hushirikishana kwa nadra sana uzoefu na uelewa wao wa maisha. Hata hivyo uelewa kwamba wanamiliki unatupatia mwangaza katika akili zetu maamuzi ya kujenga dunia iliyo ya haki zaidi, yenye uchumi imara inayoheshimu utu na mazingira ya dunia.

.Hebu tujifunze namna ya kuwasikiliza, kwa sababu maisha yao ya leo yanaweza kuwa majaliwa yetu ya kesho.

Hivi karibuni Barclay alitambua kwamba anakabiliana na tishio linguine linalotikisa dunia: virusi vya korona. Hakusita kwa muda mrefu. Alijua wapi pakwenda kuzungumzia hili: Uwani kwa ATD Dunia ya nne! Hapa ni mahali alipokuwa anakutana na vijana wengine: wale wanaoendeleza matendo ya kitamaduni katika maeneo ya hali ya chini na vijijini ambao pia pato lao ni la siku kwa siku. Kama alivyo yeye, hapo hupata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na kujifunza kutoka kwa kila mmoja.

CAR, 2020, Uwani kwa ATD Dunia ya Nne, Bangui, mradi wa Covid-19© ATD Quart Monde

Uwani kwa ATD Dunia ya Nne, Bangui, mradi wa Covid-19.

  • Pamoja na wafanyakazi wa kujitolea wa ATD, vijana hawa waliamua kwamba hawatasimama wakiangalia tu. Kirusi hiki kinamtisha kila mtu na wasipozielewesha jumuiya maskini, wakazi watashindwa kujilinda. Hivyo walikwenda kuzungumza nao wakichukua vipeperushi vinavyotoa taarifa, vituo vya kuoshea mikono vinavyoweza kutembezwa pamoja na sabuni.

Barclay aliendelea na mizunguko yake ya kukusanya takataka. Kwa sasa anatumia muda mrefu kwa sababu anatumia sehemu ya muda wake kuwaelekeza watu namna ya kujikinga dhidi ya virusi. Kila mtu anaweza kusoma na kuona hatua za kujikinga alizochora katika mkokoteni wake.

Ukitaka kufahamu zaidi angalia ATD Fourth World in Central African Republic.

0 comments Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *