MPAKA DENI LITAKAPOLIPWA

Picha © Guillermo DIAZ/AR0201602040

Baada ya kupitia changamoto nyingi, kwa pamoja Sophia mwanaharakati wa ATD kutoka maeneo ya Boko Dar es Salaam Tanzania, Hemed na Micol wafanyakazi wa kujitolea muda wote ATD, waliamua kuandika yale waliyoyapitia, kumrudishia Peresia thamani yake kwa simulizi ya ukosefu wa haki.

‘’Ninapenda kuchukua fursa hii kusimulia mkasa wa dada yangu Perisia, ambaye sasa hivi hatunaye tena hapa duniani.

HAJA YA HARAKA YA MATIBABU

Alikuwa na umri na wa miaka 37 nilipompokea katika kituo cha mabasi Dar es Salaam. Alikuwa anaumwa sana na hata sikuweza kumtambua kwa haraka. Ilikuwa ni vigumu sana kuja nae nyumbani hasa kwa kutumia usafiri wa umma. Hivyo ilinilazimu kumpeleka moja kwa moja hadi hospital iliyokuwa karibu.

MATIBABU NA MADENI

Kutokea hapo, alihamishwa hospitali mbalimbali mpaka pale madaktari waliposema kwamba upo umuhimu wa kumfanyia operesheni ya utumbo mkubwa haraka iwezekanavyo. Hata hivyo kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano (1,500, 000/= TZS) kilihitajika kilipwe kabla ya kuanza kupatiwa matibabu ya operesheni.

Nchini Tanzania, sera ya Afya humlazimu kila mwananchi kugharamia matibabu na idadi kubwa ya watu hawana bima za afya hivyo ni vigumu kumudu gharama za matibabu. Kutokana na hali hiyo inawawia vigumu baadhi ya watu kufika kwenye vituo vya Afya na kupata matibabu kwa ufanisi.

Licha ya operesheni kutakiwa kufanyika kwa haraka, nilifanya jitihada za kuwaelezea ofisi za ustawi wa jamii kuhusu hali yetu ya kiuchumi kupitia barua ya maandishi ili kuweza kupata msamaha wa kutolipia matibabu lakini hospitali haikukubali kumpatia matibabu.

Kutokana na hali hii, muuguzi aliamua kumpa Peresia namba ya mfanyakazi wa ustawi wa jamii ili ajaribu kupata ufumbuzi. Baada ya hapo afisa wa ustawi wa jamii alikwenda kumtembelea Peresia hospitali. Tulimuelezea tatizo linalotukabili, hivyo aliweza kufanyiwa operesheni na kutakiwa kulipa baada ya hapo. Kitu ambacho sio cha kawaida kufanyika kwa hapa Tanzania. Tangu hapo tukawa tunakabiiwa na deni

Peresia alipaswa kufanyiwa upasuaji mapema kabla ya kufikia hali hii lakini upasuaji ulicheleweshwa mno, kwanini walishindwa kumfanyia mapema?

Baada ya upasuaji Peresia alipata maumivu makali. Aliamka usiku mara kwa mara na kuanza kupiga kelele. Wakati mwingine majirani zetu waliamshwa na kelele na kuuliza nini kilichokuwa kinaendelea. Tulijaribu kutumia dawa za mitishamba kwa sababu hatukuweza kumudu zilizopo.

Tulilazimika kurudi tena hospitalia ambako waligundua kwamba upasuaji ulikuwa haukufanyika vizuri. Daktari aliyemfanyia upasuaji alikuwa bado katika kipindi cha mafunzo. Ikagundulika kuwa walikuwa wamekata kitu ambacho hawakupaswa kukata na Peresia kulazimika kuwa na tundu kwenye sehemu ndogo ya tumbo kwa ajili ya kutolea haja kubwa. Peresia alifanyiwa upasuaji kwa mara ya pili ili kuondosha tatizo lilijitokeza kwenye upasuaji wa mara ya kwanza. Hata hivyo madaktari waligundua kuwa tatizo la saratani lilikuwa limesambaa, hivyo waliamua kumfanyia upasuaji kwa mara ya tatu. Nilijaribu kupaza sauti yangu kuonesha hospitali wajibu wao ni upi, hata hivyo ilikuwa ngumu kupambana na mfumo uliopo.

Baada ya upasuaji wa mara ya tatu, tulikuwa tunalazimika kulipa kiasi cha shilingi milioni tatu na laki nane za kitanzania (3,800,000) sawa na Euro 1,700. Juu ya ushahidi, nilirudia mara kadhaa kuelezea hali yangu ya kiuchumi, ili kuonesha kwamba ni jinsi gani haikuwa rahisi kwa mimi na dada yangu kumudu kiasi hicho cha gharama; tulikuwa na watoto saba na kipato chetu hakikuwa cha uhakika.

KUZUIWA KUTOKA HOSPITALI NA MADHARA YAKE

Siku moja, Daktari alikwenda chumbani kwa Peresia na kumwambia kuwa anaweza kuruhusiwa na kurudi nyumbani, lakini uongozi wa hospitali uliendelea kusisitiza kuwa haiwezekani Peresia kuruhusiwa kurudi nyumbani mpaka pale deni litakapokuwa limelipwa.

Hivyo basi, siku hiyo nilirudi nyumbani peke yangu na kwenda kwa kiongozi wa serikali ya mtaa ambaye alinikutanisha na mbunge na kuweza kumuelezea yanayotukabili. Pamoja nae tulimtembelea Peresia hospitali na kuonana na uongozi ambao ulionekana kuwa mtiifu mbele ya kiongozi na kukubali kuwa utamruhusu Peresia , lakini dada yangu aliendelea kuwa chini ya ulinzi wa hospitali na hakuna kilichofanyika.

Siku chache baadaye, mkurugenzi wa hospitali na baadhi ya watu kutoka ustawi wa jamii walimtembelea Peresia katika chumba alichokuwa amelazwa na kumtamkia maneno ya kashfa kama vile “Huoni aibu kukosa pesa ya kulipia gharama ya matibabu hali ya kuwa una mikono miwili ya kufanya kazi, ikiwa kila mtu anaomba msaada, namna gani hospitali itaweza kujiendesha?” Walifanya hivi kama adhabu kwangu kwa sababu hawakufurahishwa na kitendo cha mbunge kutembelea.

Peresia aliendelea kuwa chini ya ulinzi wa hospitali kwa kipindi cha miezi mitano, watoto waliendelea kuathirika na hii hali. Kipindi chote chote hiki haikuwa rahisi kwa watoto kuonana na mama yao kwa sababu hospitali haikuwaruhusu. Hali hii ilipelekea madhara makubwa katika familia. Watoto walikwama. Kutokana na hali hii, ilikuwa inanilazimu kutumia mwendo wa masaa mawili kila siku kwenda hospitali kwa ajili ya kumpelekea chakula Peresia. Nililazimika kumuomba mwanangu mkubwa aliekuwa na umri wa miaka tisa kubaki nyumbani kuwaangalia wenzake ambao ni wadogo hivyo kumsababisha asiweze kuhudhuria shule. Mara kadhaa uongozi wa shule ulinipigia simu kuuliza kwanini mtoto haudhurii shule, wakaniambia kwamba endapo mtoto haudhurii shule mara kwa mara itanilazimu kulipia kiasi cha shilingi elfu hamsini (50,000) kama adhabu.

Kuna wakati nililazimika kulala hospitali, sababu sikuweza kumudu gharama za nauli kwenda na kurudi kila siku, hata hivyo kuna wakati walinzi wa hospitali walinifukuza mimi na baadhi ya watu wengine waliokuwa na changamoto kama zangu. Ilinilazimu pia kuzunguka huku na kule kwa ajili ya kupata mahali pakulala

Nilizunguka sehemu nyingi tofauti kwa ajili ya kutafuta kazi ili kukidhi mahitaji ya familia. Kuna wakati ilikuwa ni vigumu sana kulala hospitali, kufukuzwa na walinzi mara kwa mara, watoto kubaki peke yao nyumbani kwa muda mrefu na kupelekea kuanza kupita majumbani kuombaomba. Kuwaona watoto wangu kati hali ya kuombaomba kwangu yaikuwa ni maumivu makubwa sana.

Kipindi hiki cha miezi mitano, baadhi ya madaktari walikuwa wakimdhihaki Peresia. ”Unafanya nini hapa” walimuuliza hivi mara kwa mara. Wakati mwingine dada yangu alinipigia simu na kuniambia kuhusu mambo mabaya waliyokuwa wakimfanyia. Alitakiwa kutoendelea kutumia tena kitanda na kulala sakafuni, aliamishwa kutoka chumba kimoja kwenda kingine katika namna ambayo sio nzuri. Kuna wakati nilishindwa kumtembelea hospitali kwa sababu ya changamoto ya nauli. Hivyo kupelekea kuleta matatizo kati yangu na yeye sababu alichoshwa na madhira anayokuwa anayapitia hospitali. Kuna nyakati angeweza kunitolea maneno ya ukali, nilijaribu kuwa mtulivu, nafahamu magumu aliyokuwa anayopitia.

Kuna siku hospitali iliniruhusu kulala na dada yangu, nilipokea simu kutoka kwa jirani akiniambia kuwa Ibu mtoto wa Peresia mwenye umri wa miaka miwili (2) hakuwa amerudi nyumbani. Peresia alipiga kelele kwenye vyumba vya hospitali huku akisema napitia changamoto hizi kwa sababu ya umaskini. Daktari alisikia kelele hizi na kutujia. Peresia alichukua nyaraka na kumuelezea Daktari. Tumefanya jitihada zetu zote tunazoweza laikini bado hatutendewi kama binadamu, tumekabidhisha nyaraka zote zinazothibitisha kuwa ni vigumu kwetu kuweza kulipa deni linalotukabili. Daktari alitingisha kichwa na kusema; ‘’Nimekuelewa, changamoto iliyopo ni kutoka kwenye uongozi wa hospitali. Unaweza angalau kulipa sehemu ndogo ili kuwaonesha nia yako njema?’’ Peresia alijibu, kama ningeweza kulipa, ningekuwa nimefanya hivyo tayari. Sitaki kuendelea kukaa hapa, umeweza kuona nyaraka nilizo nazo ni vigumu hata kulipa hicho kidogo.

Siku iliyofuata daktari mwingine aliniuliza, unaweza kulipa angalau kiasi cha laki moja 100,000 ili uweze kuruhusiwa? Sikuweza kuamini, Peresia aliulizwa pia vivyo hivyo, Daktari alionekana mwenye haraka akitaka pesa itumwe kupitia namba zake za simu. Sikumuamini, sikujua nini cha kufanya. Niliamua kutuma pesa kwa rafiki wa Peresia anayelala naye chumba kimoja na kumpa maelekezo Peresia atoe pesa na kumpatia daktari ambae alionekana kutofurahishwa na nilichokifanya. Daktari alisema niende na kiasi hiko cha pesa kulipa kwenye uongozi na kupatiwa stakabadhi ya malipo, hata hivyo nilichanganyikiwa kuona hakuna kilichobadilika, Peresia aliendelea kuzuiliwa hospitali wakati huo nikiwa na deni la kiasi cha shilling laki moja 100,00 ambalo riba yake ni kiasi cha shilingi laki tatu 300,000.

KUTOA NILIYONAYO MOYONI

Siku moja nilialikwa kwenye mkutano wa marafiki wa ATD, Kupitia jirani yangu ambaye naye ni rafiki wa ATD. Niliamua kupitia tukio hili ndio sehemu ya kutoa hasira zangu mbele ya kila mmoja kuhusu hali au kadhia anayokutana nayo dada yangu. Kwa haraka niligundua kwamba watu walionizunguka pale walinipa heshima ya hali juu mno, walinipa nafasi ya kuzungumza mpaka mwisho. Baada ya kikao kumalizika Hemed na Micol walikuja kuniuliza maswali ili kuweza kufahamu tatizo kiundani zaidi, siku chache baadae walikuja kunitembelea nyumbani kwangu, kutokea pale nilipata tumaini jipya sikuwa tena peke yangu.

Siku nilipokwenda hospitali pamoja na Hemed na Micol bado ipo kwenye kumbukumbu zangu. Nilizoea kwenda hospital peke yangu na mara nyingi wakati wa kwenda hospitali nilikuwa ni mtu mwenye msongo wa mawazo kichwani mwangu. Tulipowasili hospitali nilijihisi mwenye nguvu kukabiliana na watumishi wa hospitali. Kwangu binafsi ilikuwa siku ya kipekee, na sio kwangu tu, hata kwa dada yangu pia. Tulipofika chumbani kwa Peresia aliniuliza ‘’hawa ni kina nani? baada ya kumuelezea, Peresia aliendelea kusema nafikiri hawa ni marafiki wazuri kwa sababu hawako hapa kujaribu kupata ufumbuzi wa tatizo tu, ila zaidi kwa namna ambavyo wamejitolea muda wao kunitembelea. Pamoja nao tutaishinda vita hii.’’

Pamoja nao tulionana na mkurugenzi wa hospitali na kumuelezea hali halisi ya familia yangu tena na kumuomba kuweza kupata ridhaa yake. Uongozi wa hospitali ulituona kuwa na hatia kwa sababu ya kushindwa kulipa deni. Mkurugenzi aliendelea kusisitiza kwamba Peresia hatoruhusiwa kutoka hospitali mpaka pale deni litakapokuwa limelipwa huku akiendelea kurudia tena kwamba deni lazima lilipwe ili hospitali iweze kujiendesha.

Nilijibu kwamba kuna watu wanatoka kwenye hali tofauti; baadhi wanaweza kulipa, wengine hawawezi kulipa, kama ambavyo tumejielezea mara nyingi. Licha ya maelezo yangu, mkurugenzi aliendelea kushikilia msimamo wake wa deni kulipwa. ‘’ kiasi gani ambacho unacho hapo? Nilimjibu kuwa sina chochote. Baada ya hapo yalifuata majadiliano ya muda. Baada ya masaa kupita nyakati za jioni, mkurugenzi alikubali kumruhusu dada yangu iwapo nitakuwa tayari kulipa kiasi cha shilingi laki tano 500,000/= kwa kulipa kiasi cha shilingi Elfu thelathini 30,000/= kwa mwezi.

Sikuweza zuia furaha yangu baada ya kupokea taarifa hii, kwa haraka nilikimbia kuelekea chumbani kwa Peresia na kumwambia ajiandae kuondoka, hakuweza kuipokea taarifa hii mara moja. Baada ya kutambua kwamba muda wa kuruhusiwa umefika kweli, alilipuka kwa furaha na kwenda kuwaaga wauguzi na madaktari waliokuwa wakimpatia msaada kwa kipindi chote cha miezi mitano yenye mateso.

Tulikwenda ofisi za ustawi wa jamii, kuacha kitambulisho kama dhamana kuhakikisha deni linalipwa. Hawakuonekana wenye furaha kama ambavyo nilijawa na furaha, walionekana kuchanganyikiwa kwa kuwa wameshindwa vita.

Ninaendelea kujiuliza; mimi sina elimu ya kutosha, sio daktari, lakini kwa wale wote walio katika mamlaka, waliosoma, wanajisikiaje kwa hali ya dada yangu na wale wote waliozuiliwa hospitali? Hizi taasisi ndio sababu wakati mwingine kupelekea watu kuingia katika matatizo wanayoyatengeneza. Kama nilikabiliana na matatizo mengi ni kwa sababu ya hizi taasisi zilizo na maamuzi ya kusikitisha.

Ustawi wa jamii wanapaswa kusaidia wale wote waliokatika uhitaji, lakini wao wakati mwingine wamekuwa sababu ya kuleta matatizo zaidi; jinsi wanavyowakaribisha watu ni vigumu kuvumilia, wako mbali na hali zetu halisi. Wako pale kwa ajili ya kuwakilisha taasisi wanazozitumikia, kiukweli hawatimizi majukumu yao ipasavyo.

Maisha nje ya hospitali yalikuwa na changamoto nyingi; tukiwa kwenye gari kuelekea nyumbani, usiku ule wa kwanza Peresia na mimi tulijadiliana kuhusu matamanio na ndoto zetu kwa mustakabali wa hapo baadae, hata hivyo hakuna mpango hata mmoja ulioweza kukamilika. Peresia aliendelea kuumwa, Daktari alishauri kuwa awe anakula vyakula maalumu, hivyo haikuwa rahisi kufuata utaratibu huo kwa kuwa haikuwa rahisi kumudu gharama za aina ya vyakula vilivyopendekezwa. Hivyo aliendelea kula vyakula ambavyo hakuwa anapaswa kula.

Peresia alienda mitaani kuomba kwa kujificha ili mimi nisijue. Hatukuweza kufuatilia ushauri wa kitaalamu hospitali kwa sababu ya gharama za nauli kutembelea licha ya kwamba iliahidiwa suala la kufuatilia maendeleo yake lisingekuwa na gharama za ina yoyote. Mara ya kwanza tulipotembelea hospitali kwa ajili ya mandeleo tuliombwa kulipia. Hivyo tuliamua kuacha kufuatilia maendeleo yake.

GHARAMA YA UTU

Kuna muda Peresia aliamua kuaondoka na kwenda kuishi kijijini kwetu. Nilijawa na huzuni kuona Peresia anarudi kijijini. Aliniambia “Umepitia matatizo kwa sababu yangu, umejilimbikizia madeni mengi kwa sababu ya hali hii. Changamoto zisizokwisha, ningependa kukupa nafasi japo na wewe upumzike’’.

Nilijaribu kumbembeleza lakini haikutosha kumfanya abaki, hatimae aliondoka. Baada ya miezi miwili, afya yake iliendelea kuzorota, alienda kumuona daktari na kushauriwa arudi Dar es Salaam, lakini alikataa kufuatia changamoto alizopitia huko nyuma na alifariki akiwa na umri wa miaka thelathini na tisa (39).’’

Licha ya kifo cha dada yake, Sophia anaendelea kulipa deni alilonalo hospitali huku wakiendelea kushikilia kitambulisho chake cha uraia kama dahamana. Bado yuko chini ya shinikizo kulipa deni. Alilazimika kukopa kiasi cha shilling laki mbili (200,000/=) kutoka kwa jirani kwa kutoa chumba chake kimoja na eneo lake kama dhamana. Kwa Sofia, limbikizo la madeni wakati wa matibabu ya dada yake bado unaendelea.

0 comments Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *