Suala la Kupambana NA Umaskini Uliokithiri Halina Mwisho NI Suala la Kila Siku Kwa Kisangani

Kisangani Smith Group

Ujio wa wanachama wa ATD Dunia ya Nne hapa Mkoani Njombe,

Awali ya yote Kikundi cha Kisanga Smith Group Youth Training Center, tungependa kutoa shukrani zetu za dhati kwa washirika wetu wa Timu ya ATD Dunia ya Nne. Wamefanya jambo kubwa  kihistoria kwa kutuongezea nguvu, baada ya kutuletea Salehe Seif na Salma Mosha pamoja na familia yao kuja kuungana nasi hapa Njombe. Waliungana nasi tangu mnamo tarehe 31 December mwaka jana 2020 wako hapa na sisi tukishirikiana katika shughuli zetu za kila siku na tunategemea kuwa nao pamoja kwa zaidi ya miaka miwili. Tunashukuru sana kwa kutuamini na kuunga mkono juhudi zetu katika mkoa wetu huu wa Njombe, ujio wao utatuwezesha kushirikishana maarifa, kujifunza kwa pamoja kutokana na mbinu mbalimbali katika harakati zetu za kupambana na umaskini uliokithiri. Uwepo wao tayari tumeona kunamabadiliko mazuri ndani ya Kisangani, wameshaanza kushirikiana katika usimamizi wa kazi za Kisangani kule Njombe na Mkiu, lakini pia harakati zetu za ATD zimeimarika zaidi.

Shughuli za Uhunzi

Kutokana na kuwa na shughuli nyingi huku shambani Mkiu, shughuli za uhunzi kule Njombe nimewaachia vijana wangu waendeleze shughuli hizo za uhunzi. Vijana wa Kisangani wanalitambua suala la kupambana na umaskini, vijana wangu wanaendelea kuwakaribisha vijana wengine waje kujifunza ili waweze kujiajiri wenyewe na kupunguza makali ya ajira. Kwahiyo sinashaka na vijana wangu wanahamasa ya kuendeleza shughuli za uhunzi tumeweka wazi kwa kila kijana anaetaka ama kuhitaji kupata mafunzo anakaribishwa. Kituo cha Kisangani tuko tayari kujitoa tunahakikisha kuwa vijana wenye kiu ya kupata ujuzi wanafundishwa bure.

Shughuli za Kilimo cha Maparachichi

Kilimo cha Maparachichi ni kilimo kilicholeta tija sana, kwa maana hiyo nimeona wanajamii wengi wamehamasika na kilimo hiki na wamepata mwitikio mkubwa mno. Hivyo basi sisi kama Kisangani tumeona sasa tuandae miche kwa wingi ili wale wakulima wadogo wadogo wanaoishi katika umaskini waweze kugaiwa miche bure ili na wao waweze kupanda miche kadhaa wa kadhaa kwenye mashamba yao. Na ugawaji wa miche utakuwa kuanzia miche mitano ama sita kwa kuanzia kwa zile familia zinazoishi katika umaskini uliokithiri ndizo tunazozilenga hasa. Kwa mwenye uwezo anaweza akachukua idadi ya kutosha hata hecta moja ama zaidi itategemea uwezo alionao kiuchumi. Kipao mbele chetu ni kwa familia zisizojiweza na tutahakikisha wao ndio wanakuwa wa kwanza kupata miche walau miche mitano ama sita kwa kuanzia ili wajikwamue kutoka kwenye umaskini uliokithiri.

Jambo jingine tunalolitilia mkazo ni kuhamasisha jamii zinazotuzunguka ziweze kufika kwenye eneo letu hili la shamba darasa ili waweze kuona shughuli mbalimbali zilizopo hapa na waweze kujifunza shughuli mbalimbali ambazo wanaweza kuziendeleza kwenye makazi na maeneo yao wanayoishi.

Mradi chuma

Mradi huu kwa Kisangani umeupa kipao mbele sana kwa sasa kwa sababu mradi huu utafungua fursa kubwa kwa taifa letu hasa kwa vijana niliowafundisha kazi ya uhunzi, wanaweza kuendelezwa kwenye kazi kubwa ya uyayushaji wa chuma na vijana wa jamii mbalimbali wataweza kujikita katika mradi huu. Kwa vile katika maeneo haya ya Ludewa Mwenyezi Mungu ametujaalia kuna chuma kwa wingi sana na maeneo mengi yanayoizunguka Ludewa na Makete chuma kinapatikana kwa wingi.

Kwa hiyo iwapo vijana watapewa teknologia ambayo mimi Reuben Mtitu nimeanza kufikiria na kufanya majaribio kadha wa kadha, nafanya juhudi za kubuni njia bora itakayoleta mafanikio kwa vijana wengi na kupata ajira katika shughul za kuyayusha chuma. Iwapo mradi huu utafanikiwa vizuri basi itakuwa sehemu ya vijana kujipatia kipato na kujikwamua kutoka kwenye umaskini uliokithiri. Pia vijana wengi ambao wanamaliza vyuo vikuu wanaweza kuja kujifunza na kuwa wajasiriamali kwenye uzalishaji wa matirio ya chuma na kutengeneza zana mbalimbali za kilimo na za ujenzi ili pia serikali inufaike na ukusanyaji wa mapato ya kodi katika mradi wa chuma.

Mradi wa samaki

Kwa bahati nzuri hapa shambani kuna miradi mingi.Kuna mradi wa matunda ya maparachichi mradi ambao watu wengi wanaufahamu pia tuna mradi wa chuma na mradi wa ufugaji wa samaki, kwa hiyo tunatoa wito kwa watu waje kutembelea, wanapokuja hapa watakuwa na uchaguzi kuona ni mradi upi utakaowavutia. Hivyo sasa hii ni fursa kwa jamii kuja kujifunza mimi nahamasisha jamii si jamii ya Wilaya ya Ludewa tu bali ni nchi nzima waje waangalie fursa na tujifunze kwa pamoja. Ninaamini kila mahali maji yapo na pia ardhi ipo ya kutosha, kwa hiyo ni natumaini iwapo watu watafika hapa na kujionea, kila mmoja anaweza kuona ni mradi upi utamfaa kulingana na eneo analotoka.

Karibuni Njombe karibuni Mkiu Reuben Mtitu

1 comments Leave a comment
  1. Tunawapongeza ATD fourth world kwa jitihada zenu za kupambana na umasikini tunajifunza kupitia taarifa hizi juu ya kupambana na umasikini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *