HATIMA GANI YA BAADAYE NINAYOHITAJI KWA MAKTABA YANGU YA MTAA?

street library tanzania

Programu ya Maktaba ya Mtaa Tandale ni shughuli kongwe kuliko shughuli zote za ATD Dunia ya Nne Tanzania. Ilianza miaka ishirini iliyopita mahali ambapo familia kadhaa zinaishi katika umaskini uliokithiri. Programu hii ilianza kama namna ya kuwa karibu na familia za Tandale, ili kuweza kutambua familia zilizo katika mazingira magumu katika eneo hilo hivyo kujenga mahusiano ya karibu zaidi na watu wa eneo hilo.

Tathmini ya Maktaba ya Mtaa

Mwaka 2021, ATD iliamua kufanya tathmini ya Maktaba ya Mtaa katika eneo la Tandale ili kuweza kufahamu vema ufanisi wa programu kwa ajili ya kuiboresha. Lengo la tathmini hii lilikuwa ni uhitaji wa kuelewa na kupata maoni ya wanajumuiya katika eneo hilo.

Matokeo ya tathmini hii yatatumika pia kuhamasisha uanzishwaji wa shughuli zingine za ATD.

Tathmini hii ilitekelezwa na kamati iliyohusisha wanaharakati wawili wa ATD kutoka Tandale, marafiki wawili wa ATD pamoja na wana ATD wawili ambao ni wafanyakazi wa kujitolea wa ATD timu ya Tanzania. Kamati hii ilihusisha watu kutoka katika nyanja tofauti za maisha. Wote wakiwa na ujuzi wa kutosha kuhusu Maktaba ya Mtaa katika eneo la Tandale aidha katika kuratibu ama kwa kuishi katika eneo ambalo programu ilikuwa inafanyika. Kamati ilitekeleza kazi yake kwa kufuata misingi shirikishi ya taratibu za ATD kwa kuwasikiliza watu waliokuwa wanahusika na suala hilo bila kuingilia maamuzi yao. Kila mshiriki alichangia katika sehemu zote za tathmini na kila mchango uliotolewa ulithaminiwa.

street library tanzania
Tamasha la kujifunza

Kuanzia Februari hadi August 2021

Tathmini ilifanyika kwa muda wa miezi sita kuanzia Februari hadi August 2021. Kulikuwa na jumla ya mahojiano 27 yaliyofanyika katika mtindo wa vikundi rika. Vikundi rika hivi, vilihusisha watoto wa Maktaba ya Mtaa hasa wale waliokuwa wahudhuriaji wa mara kwa mara, wawezeshaji katika programu hiyo, na wazazi wa watoto waliokuwa wanajihusisha na Maktaba ya Mtaa. Washiriki katika vikundi rika walihojiwa ili kupata maoni yao kuhusu: Maktaba ya Mtaa ilikuwa na maana gani kwao, ni kwa namna gani walifaidika na programu hiyo, ni changamoto gani walikabiliana nazo pamoja na mapendekezo ya namna ya kuiboresha.

“Kupitia programu ya Maktaba ya Mtaa, tumejifunza maana ya upendo, na kuheshimiana.”

Mtoto wa Maktaba ya Mtaa

Mwezeshaji mmoja alisema: “Wawezeshaji wengi wa sasa walikulia Tandale na walishiriki katika Maktaba ya Mtaa walipokuwa watoto.”

“Tulilelewa na wawezeshaji waliopita. Nilikuwa mtoto bado walipokuja kutusomea hadithi, hata mimi nilitaka kuwa kama wao siku moja.”

Matokeo

Tathmini ilipendekeza kwamba wawezeshaji wapate mafunzo ili kuiwezesha maktaba kufanyika kwa ubora zaidi.

street library tanzania
Tamasha la Kujifunza 2022

Suala lingine lililoibuliwa na tathmini ni eneo inapofanyika Maktaba ya Mtaa. Katika msimu wa mvua, wakati mwingine mifereji hufurika. Inapotokea hivyo, bahati mbaya watoto wanaweza kukanyaga maji machafu.

Watu wanaoishi Tandale walipendekeza kwamba eneo la Maktaba ya Mtaa liboreshwe na kupendezeshwa.

Wazazi wanaohusika na Maktaba ya Mtaa, pia walizungumzia suala la shule za serikali. Katika mahojiano, wengi wao walisema kwamba familia zinazoishi katika mazingira magumu watoto wanashindwa kupata elimu bora katika mfumo wa shule za serikali. Idadi ya watoto wanaoacha shule katika eneo la Tandale ni kubwa hususani katika eneo ambapo Maktaba ya Mtaa inafanyika. Zipo sababu kadhaa zinazosababisha, kama vile gharama ya sare za shule, vifaa vya kujifunzia, mitihani na aibu wanayoweza kukabiliana nayo waathirika wa ukimwi. Hii inahitaji umuhimu wa kufikiria kwa makini zaidi kuhusu hali ya kila mtoto na uhitaji wa msaada kwa watoto na vijana wanaoacha shule katika eneo la Tandale. Tathmini ilipendekeza kwamba ATD ianzishe programu ya kufundisha masomo ya ziada ili kuzuia watoto wasiache shule. Hii itawasaidia wale walioacha kurejea tena shuleni au kuondoka mitaani.

Tathmini pia ilielekeza mtazamo wake katika kiwango kikubwa cha watu wanasiojua kusoma na kuandika katika eneo la Tandale hali ambayo pia inaweza kuwa chanzo cha aibu kwa watu hao. Baadhi ya wazazi walipendekeza ATD irudishe madarasa ya elimu ya watu wazima ambayo hapo awali yalikuwa wanaendeshwa na shirika katika kutatua tatizo hili.

street library tanzania

Kamati ilihitimisha kwa kusema kwamba ukosefu wa miundo mbinu na huduma za afya ilikuwa sababu ya ongezeko la umaskini katika eneo hili la Tandale.

Uwasilishaji na hatima ya baadaye

Mnamo mwezi Mei 2022, ATD iliwasilisha matokeo ya tathmini katika Tamasha la Kujifunza la mwaka huo lililofanyika katika eneo lile lile la Maktaba ya Mtaa. Wakati wa tamasha, ATD ilifanya warsha tatu zilizokwenda sambamba na tathmini: sarakasi, kuchora graffiti katika kuta na klabu ya usomaji iliyoongozwa na mwandishi wa vitabu vya watoto.

Picha zaidi za Tamasha la Kujifunza mwaka 2022

Tathmini ilikuwa fursa muhimu kwa jumuiya iliyohusika katika programu ya Maktaba ya Mtaa kukutana na kushirikishana wasiwasi pamoja na matumaini yao kwa hatima ya baadaye. Ilichochea mawazo mapya ambayo yatasaidia katika mapambano dhidi ya umaskini. Tathmini pia ilionesha kwamba umaskini unaweza kushughulikiwa vizuri pale watu wanaotoka katika nyanja tofauti za maisha wanaposhirikishana mawazo yanayoheshimiwa na wote na kutekelezwa. Vilevile ilikuwa fursa ya kutafakari kwa mapana juu ya wana ATD, shirika pamoja na shughuli zake Tandale na kinachofuatia baada ya hatua hiyo.

Pakua ripoti ya tathmini

0 comments Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *